KIVUKO KIPYA CHA MV. MWANZA CHATOSWA KWENYE MAJI TAYARI KWA MAJARIBIO

News Image

Posted On: June 21, 2018

Wakazi wa jiji la Mwanza mapema leo wameshuhudia tukio la kushushwa kwenye maji kwa Kivuko kipya cha MV. Mwanza baada ya kufikia hatua za mwisho za kukamilika kwa ujenzi wake. Tukio hilo lilishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametoa pongezi kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa kusimamia mradi huo kwa mafanikio makubwa. Aidha, ameipongeza Kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Boatyard Ltd ya jijini Mwanza kwa kujenga kivuko hicho kwa ubora wake.

Kaimu Mkurugenzi wa Ukodishaji Mitambo na Huduma za vivuko kutoka TEMESA, Mhandisi Lukombe King’ombe ambaye alimuwakilisha Mtendaji Mkuu wa TEMESA alisema ni faraja kubwa kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza kupata kivuko kipya kwani kitapunguza adha ya foleni ndefu kwa watumiaji wa vivuko vinavyotoa huduma kati ya Kigongo na Busisi. Mhandisi King’ombe aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kuhakikisha kuwa wakazi wa mkoa huo wanapata huduma ya usafiri yenye uhakika na kuwataka wakazi hao kukitunza kivuko hicho kitakapoanza kutoa huduma ya uvushaji wa abiria na magari. Alisema, hatua inayofuata baada ya kivuko hicho kushushwa kwenye maji ni ukamilishaji wa kazi chache zilizobaki na hatimaye kukifanyia majaribio ili kuhakikisha abiria na mali zao wanakuwa salama pindi watumiapo kivuko hicho.

Naye Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Alex William aliwaomba wakazi wa Mwanza kujivunia kivuko hicho kwa kuwa kimepewa jina la mkoa huo na hii ikiwa ni heshima kubwa kwa wakazi hao.

Kivuko hicho cha tani 250 kina uwezo wa kubeba abiria 1000 na magari 36 na kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kati ya Kigongo na Busisi mkoani Mwanza hivi karibuni.