Lindi Kitunda wapata huduma ya kivuko

News Image

Posted On: March 09, 2018

Na Alfred Mgweno -TEMESA LINDI

Wananchi wa Lindi na Kitunda mkoani Lindi leo wameshuhudia kuwasili kwa kivuko cha MV. Kitunda ambacho kitatoa huduma katika eneo hilo na kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo kati ya Lindi mjini na eneo la Kitunda ambalo kwa muda mrefu limekuwa likifikika kwa njia ya mzunguko umbali wa kilometa 80 kwa kutumia barabara. Kuwasili kwa kivuko hicho ni ahadi aliyoitoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akiwahutubia wakazi wa maeneo hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi mapema mwezi Machi mwaka jana akiwa ziarani mkoani humo.Akizungumza mara baada ya kuwasili kwa kivuko hicho Katibu wa CCM wilaya ya Lindi Bw. Stanley Mkandawile amesema hii ni faraja kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Lindi na Kitunda ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata adha kubwa ya usafiri unaounganisha maeneo hayo na amewataka kuhakikisha wanakitunza na kukithamini kivuko hicho. Bw. Mkandawile alisema serikali ya awamu ya tano imeendelea kutekeleza sera yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi.Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu alisema ujenzi wa maegesho ya kivuko cha Lindi/Kitunda umekamilika kwa asilimia 98 na ujenzi wa vyumba vya abiria unaanza mara moja.Aliongeza kusema “Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa aliwaahidi juzi (Jumatatu) kwamba kivuko hiki kitafika hapa Lindi (Jumatano) hivyo kazi yangu ilikuwa ni kuhakikisha ninatekeleza ahadi hiyo, ninayo furaha kubwa kuwaeleza wananchi hususani wa Lindi kwamba kivuko kimefika na kipo tayari kutoa huduma kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kusafiri kutoka Lindi kwenda Kitunda na vile vile kutoka Kitunda kwenda Lindi.”Aidha, Dkt. Mgwatu alibainisha kuwa kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 kwa pamoja sawa na uzito wa tani 50. Ujenzi wa maegesho ya kivuko upande wa Lindi na Kitunda umegharimu Shilingi za kitanzania Bilioni 1.97 na umefanywa na kampuni ya kizalendo ya Hematek Investment Limited.Kivuko cha MV Kitunda kimewasili jana jioni na kitaanza kutoa huduma haraka iwezekanavyo.