MKURUGENZI HUDUMA ZA UFUNDI SEKTA YA UJENZI AFUNGUA BARAZA LA WAFANYAKAZI TEMESA

News Image

Posted On: April 17, 2018

Mkurugenzi wa Huduma za ufundi sekta ya ujenzi Mhandisi William Nshama ameupongeza uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA kwa utendaji mzuri wa kazi na kuwataka kuhakikisha kwamba wanaendelea dhana ya utawala bora kwa kusikiliza na kutatua kero mbali mbali zinazoukabili wakala huo.

Mhandisi Nshama ameyasema hayo wakati akizindua kikao cha baraza la wafanyakazi la wakala huo katika ukumbi wa mikutano wa Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam. ''TEMESA imefanya kazi kubwa sana kwani tumeshuhudia ujio wa vivuko vipya katika maeneo ya Kigamboni lakini pia nimeona wakazi wa Lindi wamepelekewa kivuko na sasa wanavuka vizuri kutokea Lindi kwenda Kitunda, kwa hilo nawapongeza sana''. Alisema Mhandisi Nshama.

Aidha aliutaka uongozi wa TEMESA kuhakikisha unatatua kero ambazo mara kwa mara zimekua zikiripotiwa kutokea katika upande wa karakana.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa wakala huo Dkt. Mussa Mgwatu aliwataka wajumbe na watendaji kuhakikisha wanashirikiana katika utekelezaji wa malengo waliyojiwekea katika kuleta maendeleo ya wakala huo kwa kutoa huduma bora kwa wakati wote. Aliwataka kuhakikisha wanajipanga kufanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa kwa ustawi wa wakala na kuhakikisha wanafuatilia madeni yote ya wadaiwa sugu, ushirikishwaji wa wafanyakazi wote katika kutoa maamuzi na pia aliwaomba mameneja wote wa mikoa na vituo kuhakikisha wanaongeza mapato katika vituo vyao ili kuweza kutatua kero ndogo ndogo zinazowakabili vituoni.

Uzinduzi wa Baraza hilo ulienda sambamba na uchaguzi wa katibu wa baraza hilo ambapo Ndugu Julius Mwashamba kutoka TEMESA makao makuu aliteuliwa kuwa katibu wa baraza hilo baada ya aliyekua katibu hapo awali kuhamia ofisi nyingine.